Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
27 APRILI 2022
Kamati ya lishe Halmashauri ya Manispaa ya Songea yajipanga kuhamasisha jamii kutumia mazao lishe kwa lengo la kudhibiti utapiamlo na udumavu katika jamii.
Hayo yamebainishwa katika kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe Manispaa ya Songea kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021/2022, kilichofanyika leo tarehe 27 Aprili 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Manispaa ya Songea, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Christopher Ngonyani (Mratibu Tasaf Manispaa ya Songea), alisema kuwa kamati ya lishe imejipanga kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya maziwa kupitia vyombo vya habari pamoja na mikutano mbalimbali inayofanyika katika ngazi ya Kata na Mitaa.
Aliongeza kuwa, kupitia maadhimisho ya siku ya wakulima (Nane Nane) inayotarajiwa kufanyika tarehe 8 Agosti 2022, kamati ya lishe imejipanga kutoa elimu ya namna ya uzalishaji mazao lishe kama vile mahindi ya njano, viazi lishe na mchicha lishe kwa jamii pamoja na umuhimu wa kutumia mazao hayo katika kuboresha afya na kudhibiti utapiamlo na udumavu hasa kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5.
Ngonyani ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho lishe wanapokuwa shuleni pamoja na kuwataka wazabuni wanaosambaza chakula mashuleni kupeleka chakula chenye viini lishe hasa kutumia mahindi lishe ili kuimarisha afya za watoto hao.”Alisisitiza”
Akitoa tathimini ya utekelezaji wa shughuli za lishe, Afisa lishe Manispaa ya Songea Florentine Kissaka amesema kuwa hali ya lishe kwa Manispaa ya Songea inazingatia viashiria mbalimbalia ambapo hadi sasa idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 wenye utapiamlo mkali imefikia watoto 21 sawa na asilimia 0.2% na asilimia 6.6% ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu pamoja na asilimia 35.3% ya watoto wenye udumavu.
Kissaka ametoa wito kwa jamii kuzingatia taratibu za kiafya na utumiaji wa lishe bora zinazotolewa na wataalamu wa afya ngazi ya jamii na katika vituo vya afya ili kukabiliana na utapiamlo na udumavu hasa kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5.
Amewataka akinamama wanaonyonyesha kuzingatia maelekezo wanayopewa na watoa huduma katika vituo vya afya ikiwemo na kunyonyesha mtoto chini ya miezi 6 pasipo kumlisha chakula cha aina nyingine na baada ya muda huo kumpatia mtoto chakula cha ziada chenye virutubisho lishe ili kuepukana na tatizo la udumavu na utapiamlo.
“Miongoni mwa mikakati iliyowekwa katika kukabiliana na utapiamlo na udumavu katika jamii ni kuhakikisha ulimaji wa bustani za mbogamboga pamoja na upandaji wa miti ya matunda katika maeneo ya shule pamoja na kutoa elimu ya maandalizi ya chakula lishe shuleni” Kissaka alibainisha.
Naye Afisa kilimo Msaidizi Manispaa ya Songea Claudy Yacent Massawe alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma unafanya vizuri katika eneo la uzalishaji wa chakula ambapo hadi sasa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula inafikia Tani Laki moja na hamsini elfu ambapo Tani sitini na nane elfu pekee hutumika kwa chakula.
Massawe amewataka wakulima kujikita kwenye kilimo cha mazao lishe hasa mahidni ya njano na viazi lishe kwa lengo la kuondoa changamoto ya utapiamlo na udumavu katika jamii.
Kwa upande wake mdau wa kamati ya lishe Manispaa ya Songea Agrey Kapinga amesisitiza utoaji wa elimu kwa jamii juu ya utumiaji wa mazao yanayozalishwa kwa mfumo wa lishe bora pamoja na namna ya uandaaji wa vyakula mbalimbali kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa