MAADHIMISHO ya mashujaa wa vita vya Majimaji Mkoani Ruvuma hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 27 februari kwa ajili ya kuwaheshimu na kuwaenzi mashujaa vinara wa vita vya majimaji ambao walinyongwa na wakoloni ya wakijerumani kwa lengo la kutengua nguvu za upinzani kutoka kwa waafrika ili kuzima vita.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassimu Majaliwa (MB) ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Inocent Bashungwa (MB) iliyofanyika 27 februari 2021 katika eneo la Makumbusho ya vita vya Majimaji Manispaa ya Songea.
Mh. Bashungwa alisema lengo la Serikali ni kulinda na kutunza uhifadhi wa maeneo hayo ya kihistoria pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa maeneo hayo ya kihistoria ya urithi wa ukombozi wa Afrika.
Alisema miongoni mwa mashujaa wa vita vya Majimaji ambao walizikwa katika kaburi moja wapatao 66 kati ya hao alikuwepo mwanamke mmoja mwenye cheo cha Nduna ambaye aliitwa Mkomanile. Hivyo alitoa wito kwa wanawake wote siku ya maadhimisho ya wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 08 machi kila mwaka akumbukwe mwanamke shujaa Mkomanile ambaye alipigana vita hadi kufa. Alisisitiza.
Aidha katika ziara hiyo aliweza kutembelea kambi ya Masonya iliyopo Wilayani Tunduru iliyotumika kwa ajili ya mafunzo ya jeshi iliyotumiwa na wapigania uhuru wa chama cha FRELIMO-Msumbiji, Likuyu Sekamaganga- shule iliyotumika kutolea mafunzo kwa watoto wa wapigania uhuru Msumbiji iliyopo Wilaya ya Namtumbo pamoja na maadhimisho ya vita vya Majimaji iliyopo Manispaa ya Songea.
Naye Mhifadhi wa Makumbusho ya Majimaji Mkoa wa Ruvuma Adson Ndyanabo alisema eneo la kihistoria la Mashujaa na vinara wa vita vya majimaji wapatao 67 walinyogwa tarehe 27.02.1906 wakati wa vita vya majimaji ikiwa ni mbinu mojawapo ya Serikali kikoloni ya wajerumani na kutengua nguvu kwa ajili ya kuzima vita.
Aliongeza kuwa watu wote walioshiriki mapambano walikamatwa kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma kwa nyakati tofauti kuanzia novemba 1905 hadi 1906 na kuwekwa gerezani wakisubibili na kunyongwa ambapo kaburi kubwa lilichimbwa mwezi mmoja kabla ya siku ya kunyongwa na kazi hiyo ilifanywa na wafungwa hao”mashujaa”.
Alisema Zilisimikwa nguzo ndefu mbili na kuwekwa mwamba juu ya nguzo na kufunga vitanzi vya Kamba vinne katika mwamba na chini ya mwamba huo mkubwa zilisimikwa nguzo fupi nne na juu ya nguzo hizo fupi 2 ziliwekewa mwamba kwa juu.
Alibainisha kuwa kabla ya kunyongwa mashujaa hao walibatizwa, kisha wanyongwaji waliletwa kwenye eneo la unyongaji kila mnyongwa akiwa amefungwa mnyororo shingoni na kuvishwa kishuka kiunoni ili kufunika miili yao na kufungwa kitambaa chekundu ili wasione huku mikono yao ikifungwa nyuma ya mgongo kisha walivishwa kitanzi shingoni na kuning’inizwa vitanzi na kila kitanzi kwa mnyongwa mmoja.
Alisema siku ya kwanza walinyongwa 40 na kisha walizikwa kwa kulazwa kiubavu katika kaburi moja la alaiki la mashujaa 66 akiwemo mfalme (NKOSI) jamii ya wangoni aliyeitwa Mputa Wazerapasi Gama na kaburi la pili alizikwa Nduna Songea.
Adson alisema nguvu kubwa ya upinzani ilitokana na uongozi thabiti wa wangoni Nkosi (mfalme) na Nduna ambaye alikuwa na nafasi ya wasaidizi wa Mfalme na majemedari wa vita pia jumbe ni nafasi ya viongozi wa vijiji walioandikwa na raia walikuwa wapiganaji ambao hawakuwa na vyeo vikubwa.
Mnara huo ulijengwa 1980 kwa ajili ya kuheshimu,na kutunza mchango wao wa uzalendo wa mashujaa katika kupigania uhuru.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
27.02.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa