Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekusudia kuanzisha na kuendeleza Mpango wa pamoja (jumuishi) wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kama (ugonjwa wa minyoo ya tumbo na minyoo ya kichocho) katika Wilaya zote zilizoathirika na magonjwa hayo nchini Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa jana 15.09.2020 na Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele Manispaa ya Songea Dr. Broady Komba kwenye kikao cha Maafisa watendaji wa kata 21, Wenyeviti wa Mitaa 95 pamoja na wataalamu Sekta ya Elimu Msingi kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Broady alisema lengo kuu la Serikali ni kupunguza maradhi yatokanayo na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kiupaumbele nchini Tanzania ili kufikia kiwango ambacho si tatizo la afya kwa jamii pamoja na kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora na isiyodhoofishwa na maradhi.
Alisema Manispaa ya Songea inakusudia kugawa dawa za minyoo ya tumbo na minyoo ya kichocho kwa wanafunzi wa shule za Msingi 91 za Manispaa ya Songea, kwa idadi ya wanafunzi wapatao 58,000 kwa wanafunzi wenye umri kuanzia miaka 5-14.
Alifafanua kuwa zoezi hilo linatarajia kufanyika kuanzia siku ya ijumaa na jumatatu yaani 18-21/2020 kwa usimamizi wa walimu wakuu wa shule husika pamoja na wataalamu wa afya ili kuhakikisha dawa hizo zinagawiwa vizuri kwa kila mwanafunzi aliyeandikishwa shule hapo.
Aliwaasa Wenyeviti wa mitaa pamoja na vyombo vya Habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii/ wazazi / walezi ili waweze kuwapatia watoto wao chakula cha kutosha kabla ya kumeza dawa hizo ili ziweze kufanya kazi vizuri bila kuleta tatizo lolote.
Alizitaja faida za kutumia dawa hizo ni kuwa na mtoto mwenye afya bora, kuwa na utimamu wa akili na kuongeza ufaulu mzuri wa mtoto pamoja na husaidia kuondoa maradhi ya kifafa.
Hakusita kuzitaja baadhi ya dalili ambazo zinaweza kujitokeza kwa mtu aliyekunywa dawa hizo ni kutapika, kuhisi kichefuchefu, na kulegea lakini alisema kuwa dalili hizo zisiwatie hofu kwani hujitokeza mara chache, na tatizo likizidi mtoto huyo atapelekwa kituo cha afya kilichojirani kwa msaada Zaidi.
Aidha baada ya maelekezo hayo kwa Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Kata, yatatolewa tena maelekezo kwa Wakuu na walimu wa afya wa shule za Msingi zote ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji Zaidi.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
16.09.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa