Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
20 MEI 2022
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya kikao cha baraza la Madiwani na kupitia taarifa mbalimbali ambazo zimetekelezwa kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021/2022.
Baraza hilo limefanyika hapo jana tarehe 19 Mei 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na wataalamu, wananchi pamoja na viongozi mbalimbali.
Akizungumza katika baraza hilo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amewataka wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Manispaa ya Songea.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya 6 sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ikiwemo na ujenzi wa madarasa pamoja na vituo vya afya.
Akijibu maswali ya papo kwa papo kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa Songea Christopher Ngonyani alisema kuwa kuhusiana na ukamilishwaji wa ujenzi wa Zahanati ya Lupapila ifikapo mwezi Julai 2022 Zahanati hiyo pamoja na Zahanati ya Ruhuwiko zitaanza kutumika ambapo kiasi cha shilingi Millioni 150 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ili huduma ianze kutolewa.
Ngonyani alibainisha kuwa soko la mbao Mfaranyaki linatarajiwa kuhamishiwa rasmi katika eneo la viwanda Lilambo ambapo taratibu za kuandaa mazingira kwa ajili ya wafanyabiashara hao bado zinaendelea kukamilishwa
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amewataka Madiwani kuwahamisisha wananchi juu ya kushiriki kikamilifu katika zoezi la uwekaji vibao vya anuani za makazi kwenye Barabara pamoja na nyumba zao ambapo hadi kufiki tarehe 30 Mei 2022 zoezi hili linatakiwa kukamilika.
Mgema ametoa wito kwa Madiwani kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kuandaa taarifa sahihi ambapo zoezi hilo litafanyika Agosti 23 mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha Mapinduzi (CCM) Abdul Mkalipa amewataka viongzoi wa Halmasahuri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha wanakamilisha miradi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa wakati ikiwemo na ujenzi wa madarasa pamoja na ofisi za Serikali za mitaa.’Alisisitiza’
Mkalipa amewataka viongzoi hao kuzingatia maelekezo yanayotolewa na baraza la Madiwani hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.
Amewataka waheshimiwa Madiwani kuhakikisha wanatimiza wajibu wo kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa manufaa ya wananchi waliwapa dhamana ya uongozi.
mwisho
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa