Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15 AGOSTI 2022.
Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma na utawala bora Mhe. Jenista Joackim Mhagama ameongoza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma katika Tamasha la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ kwa shughuli za utalii na uwekezaji Mkoani Ruvuma.
Tamasha hilo limefanyika hapo jana Agosti 16, 2022 katika uwanja wa Majimaji uliopo ndani ya Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhagama ametoa pongezi kwa viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza sekta ya utalii na uwekezaji nchini kwa kuandaa tukio la tamasha hilo.
Waziri Mhagama aliongeza kuwa Filamu ya ‘The Royal Tour’ imelenga kutangaza duniani vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini Tanzania ambapo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii kutoka nje ya Tanzania na kusaidia kuongeza thamani na uchumi wa pato la Taifa kwa ujumla.”Alibainisha”
Ametoa rai kwa viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha sekta ya madini ambayo inaongoza katika ujenzi wa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma.
Waziri Mhagama amewakumbusha viongozi wote Mkoani Ruvuma kutengeneza mifumo ya kitehama kwa kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato yatakayosaidia kuboresha miundombinu ya uwekezaji.
Pia, amewataka viongozi kusimamia vyema ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya, maji na umeme ili kuleta uchochezi wa uchumi endelevu katika Mkoa wa Ruvuma.’Alisisitiza’
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alisema kuwa lengo la Tamasha hilo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuonyesha vivutio vilivyopo Mkoani Ruvuma.
Ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa ya uwekezaji iliyopo Mkoani Ruvuma ikiwemo na kilimo pamoja na kutembelea vivutio vilivyopo ikiwemo na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ziwa Nyasa, Jiwe Mbuji pamoja na chanzo cha mto Ruvuma kilichopo kwenye Mlima wa Matogoro.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitoa katika kukamilisha uandaaji wa mradi wa filamu ya ‘The Royal Tour’ ambayo imeleta mafanikio makubwa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Oddo Mbunda ameishukuru Serikali kwa kutoa Mbolea ya Ruzuku kwa wananchi wake ambayo itasaidia ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara Mkoani Ruvuma.
Tamasha hilo liliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo na kutembelea chanzo cha mto wa Ruvuma kilichopo katika Mlima wa Matogoro ndani ya Manispaa ya Songea pamoja na burudani za ngoma za asili na wasanii mbalimbali.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa