MKUU wa Wilaya ya Songea Wilaman Kapenjama Ndile amewataka Viongozi wa Serikali za Mitaa/kata kusoma taarifa ya mapato na matumizi kwa kila robo ya mwaka ili kuweka uwazi na uwajibikaji kwa wananchi wanaowaongoza.
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake, Ibara ya 145 na 146, Serikali za Mitaa ni vyombo vya wananchi ambavyo vipo katika ngazi ya chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo huundwa, huendeshwa, husimamiwa na kuwajibika kwa wananchi wenyewe ambapo huwezesha wananchi kuwa na Sauti katika maamuzi mbalimbali kwa kushiriki moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao katika shughuli za maendeleo na utawala.
Kwa kuzingatia hilo Serikali ya Mtaa kupitia Mwenyekiti wa Mtaa inao wajibu kutoa taarifa za mbalimbali za maendeleo ya mtaa husika ikiwemo na kusoma mapato na matumizi ya fedha zilizopokelewa kupitia mkutano wa hadhara kwa lengo la kuweka uwazi na ushirikishwaji jamii na endapo hatatoa taarifa ya Mapato na Matumizi anaweza kushitakiwa kwa mujibu sheria.
Hayo yamejili katika kikao kazi cha Maafisa Watendaji wa Mitaa 95, Wenyeviti wa Mitaa 95, Watendaji wa kata 21, kamati ya Ulinzi na usalama, pamoja na Wakuu wa idara na Vitengo kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea tarehe 03 Mei 2023 kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao watendaji na wenyeviti wa mitaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mhe. Ndile alisema Serikali ikitoa maagizo hayana budi kutekelezwa hivyo amewataka Viongozi hao kuhakikisha wanasimamia suala la mzazi kuchangia chakula cha shule kwa shule za msingi na Sekondari ifikapo julai 2023 kwa lengo la kuinua ufaulu wa wanafunzi.
Aliongeza kuwa ili kufanikisha zoezi hilo kila mtaa unatakiwa kuitisha vikao vya kamati za Serikali za Mtaa, mikutano ya hadhara, Bodi za shule pamoja na kamati za shule ili kuweka mkakati bora wa utekelezaji na usimamizi wa michango kutoka kwa wazazi ikiwemo na kufungua akaunti na utunzaji wa chakula.
Hali halisi ya utoaji wa chakula shuleni Wilaya ya Songea kwa Halmashauri ya Madaba ni 96%, Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni 97% ana Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni 67%. Mhe. Ndile “ Alibainisha.”
Kwa upande wake Afisa utumishi Manispaa ya Songea Sadiki Mrisho akiwakumbusha majukumu ya Wenyeviti na Maafisa watendaji wa mtaa aliserma Mwenyekiti wa Mtaa atakuwa Mwenyekiti wa mikutano yote ya kamati ya mtaa na Mkutano wa Hadhara, Msuluhishi wa migogoro midogomidogo ambayo haistahili kuitisha mikutano wa mtaa au kupeleka baraza la kata au Mahakama, kuwaongoza na kuwahimiza wakazi wa mtaa shughuli za maendeleo, kutekeleza kazi atakazopewa na kamati ya mtaa na Mkutano Mkuu wa Mtaa au kamati ya maendeleo ya kata na nyinginezo.
Aliongeza kuwa Wajibu wa Afisa Mtendaji wa Mtaa ni kuwa Mtendaji Mkuu wa Mtaa, kusimamia utekelezaji wa Sera za Halmashauri, kuishauri kamati ya maendeleo ya Mtaa kuhusu maendeleo ya Mtaa, kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo pamoja na sheria nyingine, kuishauri kamati ya mtaa kuhusu masuala ya ulinzi na usalama na nyinginezo. “Mrisho alibainisha.”
Kwa upande wake Inspekta wa Jeshi la Polisi Songea Melinda Mgumba kutoka Dawati la jinsia na watoto ni sehemu maalmu katika kituo cha Polisi inayoshughulikia Waaathirika wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na watoto kwa lengo la kutenganisha sehemu ya huduma kwa waathirika wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kumpa muathirika nafasi ya kutulia itakayomfaa ili asiendelee kudhalilika, kusikiliza maelekezo kwa usiri mkubwa, kutoa ushauri kutegemea na lalamiko lililowasilishwa, pamoja na kuchukua hatua.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Janeth Moyo alisema Manispaa ya Songee imeweka Mkakati wa utoaji wa chakula shuleni katika kipindi cha mwaka 2023/2024 ikiwemo na kuitisha vikao vya wazazi na kufanya tathimini yay a uchangiaji wa michango ya mwaka mmoja ambapo wazazi wameridhia kuchangia mahindi kilo 80 za Mahindi na Maharage kilo 24 na fedha shilingi 40,000 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mahitaji mbalimbali pamoja na malipo ya wapishi.
Aliongeza kuwa kulingana na tathimini iliyofanyika kwa kipindi cha muhula wa kwanza wa masomo kuanzia januari 2023 hadi Mei 2023 takwimu zinaonesha ni 37% za wanafunzi wa za Sekondari ndio wanaopta chakula cha mchana shulenia ambapo hupelekea kuwa na matokeo yakitaaluma yasiyoridhisha.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa