Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema, amewataka wafugaji wa mbwa kufuata taratibu za ufugaji ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea na kuathiri jamii kwa kung’atwa au kujeruhi watu au mifugo migine na kusababisha jamii kupatwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao hauna tiba bali unakingwa kwa chanjo.
Hayo yamebainishwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 28 septemba kila mwaka ambapo kwa Manispaa ya Songea iliadhimishwa katika uwanja wa Double ‘M’ uliopo kata ya Msamala Mtaa wa Mkuzo kwa lengo la kutoa tathimini ya hatua zilizofikia katika kudhibiti kichaa cha mbwa na madhara yake.
Pololet alisema Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Afya na Maliasili wanafanya jitihada katika kupunguza maambukizi ya kichaa cha mbwa kwa binadamu kwa kutoa mafunzo ya utunzaji bora wa mbwa kwa wafugaji wa mbwa na kuchukua hatua ya kuua mbwa kwa 50% wasio kuwa na wamiliki pamoja na kutoa chanjo ya mbwa.
Aliongeza kuwa kila mfugaji ahakikishe anafungia mbwa wake kwenye banda au mnyororo kwa muda wote ili kuilinda jamii inayokuzunguka na kuepuka madhara makubwa ikiwemo na kujeruhi watu, kusababisha hofu na kuwa tishio kwa jamii, kuchafua mazingira, kusambaza wadudu nyonya na kueneza ugonjwa wa kichaa cha mbwa na tegu mbwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Songea Philipo Beno Mpwessa amesema ili kudhibiti au kutokomeza tatizo la kuzurula mbwa holela Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeweka mikakati ikiwemo na kuratibu suala la mazingira kiutamaduni, kiuchumi, kijamii, kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki za wanyama, kutoa elimu juu ya ufugaji bora na udhibiti wa magonjwa ya mbwa, kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa, kuuwa mbwa wote wanaozurula na kutoza adhabu, kuwachukulia hatua wafugaji wote ambao hawajachanja mbwa wao, kutenga fedha kwa ajili ya kudhibiti kichaa cha mbwa na kuhakikisha kila mfugaji wa mbwa kuhama na mbwa wake wakati anapohamisha makazi yake.
Beno alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kuipa kipaumbele wizara ya mifugo na uvuvi kwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa chanjo ya kichaa kwa dozi 1000 ambayo imetolewa bure katika maadhimisho ya kichaa cha mbwa duniani.
Naye Dkt. Seria Shonyela alisema mwaka 2021 Manispaa ya Songea walichanja mbwa 3960 na mwaka 2022 wanatarajia kutoa chanjo kwa mbwa 4000.
Kwa upande wa wafugaji wa mbwa waltoa shukrani kwa Serikali kuadhimisha siku ya kichaa cha ambapo imewasaidia kupata huduma ya chanjo bure bila malipo yoyte, pamoja na elimu ya ufugaji wa mbwa.
Kauli mbiu ya mwaka 2022 ni; KICHAA CHA MBWA, AFYA MOJA, VIFO SIFURI ( RABIES, ONE HEALTH, ZERO DEATH)
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa