Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
02 MEI 2022.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yalianza karne ya 18 wakati wa mapinduzi ya viwanda Barani Ulaya hususani katika Taifa la Uingereza ambayo huadhimishwa Duniani kote kila ifikapo tarehe 1 Mei ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2022 Mkoa wa Ruvuma umeadhimisha sherehe hizo katika Wilaya ya Namtumbo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Ruvuma Willey Luambano alisema kuwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Mkoani Ruvuma linaundwa na muunganiko wa vyama 13 vya wafanyakazi ambapo lengo kuu la vyama hivyo ni kusimamia na kutetea haki za wafanyakazi .
Luambano alibainisha miongoni mwa changamoto inayowakabili wafanyakazi ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii kushindwa kutoa huduma bora kwa wafanyakazi ikiwemo na stahiki zao hasa wanapostaafu kazini.
Amekemea tabia ya baadhi ya vyama vya kitaalamu kukiuka taratibu na kuwa wasemaji wa wafanyakazi badala ya kuachia jukumu hilo kwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi ambao ni wasemaji husika wa wafanyakazi.
Akisoma risala ya shirikisho la vyama vya wafanyakazi Mkoani Ruvuma, Mratibu wa sherehe za Mei Mosi Mkoa wa Ruvuma Ashrafu Chussi alisema chimbuko la maadhimisho hayo ni kuwakumbuka wafanyakazi walioungana kukujinasua na ukandamizaji wa waajiri mnamo karne ya 18 kutokana na uchache wa watendaji kazi na tamaa za Wajiri kwa wakati huo kutaka kuzalisha Zaidi kwa faida zaidi ambapo wafanyakazi walifanya kazi masaa 18 mfululizo na kwa ujira mdogo.
Chussi akieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi Mkoani Ruvuma ikiwemo na wafanyakazi kutolipwa kwa wakati madeni ya uhamisho, waajiri kutopeleka malipo kwenye mifuko ya jamii kwa wakati, baadhi ya wafanyakazi kuachishwa kazi bila kufuata utaratibu, kucheleweshwa kwa malipo ya nauli na mizigo kwa wafanyakazi waliostaafu kazini pamoja na mishahara midogo inayopelekea mfanyakazi kushindwa kumudu gharama za maisha.”Alibainisha”
Aliongeza kuwa kutatuliwa kwa changamoto hizo kutasaidia wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi na ueledi zaidi kwa lengo la kuleta maendeleo kwa Taifa.
Alitoa rai kwa wafanyakazi wote kuzingatia maadili ya kazi na kujiepusha na vitendo visivyofaa kazini ikiwemo na rushwa, ubadhilifu wa mali za Serikali pamoja na uzembe kazini kwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka kanuni na taratibu za utumishi wa umma. ’Chussi alisisitiza’
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Julius Ningu ambapo alisema “mapendekezo yote yaliyotolewa na wafanyakazi kwa Serikali kuu ikiwemo na suala la nyongeza ya mishahara kwa kuwa Serikali ya Awamu ya sita imedhamilia kuboresha maslahi ya wafanyakazi”.
Amewataka waajiri kuhakikisha wanatatua changamoto ya malipo ya uhamisho kwa wafanyakazi pamoja na kuzingatia muongozo uliowekwa na Serikali katika kuzingatia stahiki za wajumbe wa vikao vya baraza la wafanyakazi kwa wakati.
Dkt. Ningu ametoa wito kwa waajiri na watumishi wote kuzingatia misingi ya utawala bora kwa lengo la kuepusha migogoro kazini baina ya muajiri na mfanyakazi kwa kufuata utaratibu wa kufanya vikao vya muundo na vya kisheria ili kubaini changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu katika maeneo ya kazi.
Amewapongeza wafanyakazi wote Mkoani Ruvuma kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya 6 katika kuleta maendeleo nchini.
Ametoa wito kwa wafanyakazi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuendelea kupata chanjo inayotolewa katika vituo vya afya pamoja na kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti mwaka huu.’Dkt. Ningu Alihitimisha’
Kauli mbiu ya Mwaka 2022; “MISHAHARA NA MASLAHI BORA KWA WAFANYAKAZI NDIYO KILIO CHETU, KAZI IENDELEE”.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa