Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe mosi 1 desemba ya kila mwaka ambapo kwa Manispaa ya Songea Maadhimisho hayo yamefanyika kata ya Lizaboni.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema yaliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa ukimwi, Wataalamu na wananchi kwa lengo la kuongeza ufahamu wa ugonjwa wa UKIMWI ambao unaosababishwa na Virusi vya UKIMWI.
Pololet alisema “ maadhimisho hayo yanalenga Kutoa fursa ya kutathmini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI kitaifa na kimataifa, Kutafakari changamoto, mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Alibainisha kuwa maadhimisho yanasaidia Kutafakari na kutekeleza kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana na vipaumbele vya kidunia na kikanda na kitaifa kwa muktadha wa kitaifa pamoja na Kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha yao kutokana na UKIMWI pamoja na kuwajali yatima waliotokana na vifo vinavyohusiana na UKIMWI na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya unyanyapaa pamoja na kupinga na kukomesha kabisa vitendo na tabia za unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI katika jamii.
Msisitizo mkubwa katika kauli mbiu hii inatukumbusha kuwa ‘’Binadamu wote ni sawa’’ hivyo mahitaji yetu sote ni sawa na tunahaki sawa kama binadamu, hivyo tunahitaji kuwa na mshikamano wa pamoja katika jamii kwenye kupinga kila aina ya viashiria vinavyokandamiza usawa na haki za binadamu pamoja na kuyafikia makundi yote ya kijamii katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wote nchini ili kuyafikia malengo ya 95 – 95 – 95 ifikapo mwaka 2025.
Naye Afisa Maendeleo ya jamii Manispaa ya Songea Martin Mtani alisema Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwenye Halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla.
Mtani alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 Manispaa ya Songea jumla ya watu 37856 wamepima afya zao, Wanaume 17273 na Wanawake 20585 kati hao Wanaume 611 na Wanawake 933 wamekutwa na maambukizi ya VVU sawa 4% wote wamefanikiwa kuunganishwa na huduma ya tiba na matunzo katika vituo vya kutolea huduma za VVU (CTC) ambapo hali halisi ya maambukizi inaonesha kushuka kwa 0.1% ikilinganishwa na mwaka wa fedha Julai 2020 hadi Juni 2021 ambapo ilikuwa ni 4.1%.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuwa na tabia ya kupima na kutambua Afya zenu kwa hiyari kila mara endapo ukikutwa na maambukizi ya VVU unaunganishwa katika huduma na tiba ya kufubaza VVU, kwa kufanya hivyo tutaimarisha afya zetu na kuimarisha kinga za mwili dhidi ya magonjwa nyemelezi.
Aliongeza kuwa ukipima na kujua huna maambukizi kunasaidia kuchukua tahadhari nakuacha tabia hatarishi zinazoweza kupelekea kupata maambukizi ya VVU.
kauli mbiu ya mwaka 2022 “Equality “imetafsiriwa kwa Kiswahili kuwa “Imarisha Usawa.”
Imeanadaliwa na;
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa