NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
20.09.2021
Katibu wa Itikadi na uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka amefanya ziara kwa muda wa siku mbili kuanzia jana tarehe 19 September 2021 na kumalizika leo tarehe 20 September 2021 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mujibu wa Ilani ya chama cha mapinduzi.
Katika ziara hiyo Shaka aliambatana na Mbunge wa jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema pamoja na viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi Wilaya ya Songea na kutembelea mradi wa machinjio ya kisasa uliopo Shule ya Tanga, Tawi la chama cha mapinduzi Mlelewa kata ya Mletele pamoja na kuzungumza na wazee kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mletele Shaka alisema kuwa chama cha mapinduzi (CCM) kitaendelea kuhakikisha kinasimamia vizuri utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitatua.
Amewataka Waheshimiwa Madiwani wote kuhakikisha wanasimamia majukumu yao kwa ueledi hasa shughuli za maendeleo kwa kuitisha mikutano mara kwa mara na wananchi ili kuwaeleza hatua mabalimbali za maendeleo kwenye kata zao, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pamoja na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati na inakuwa na thamani sawasawa na gharama zinazotumika katika kutekeleza miradi hiyo na kwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi ibara ya 225.”Shaka Alisisitiza”
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2022 chama cha mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa ndani na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya shina hadi ngazi ya Taifa.’Shaka alibainisha’
Shaka alitoa nafasi kwa wananchi wa kata ya Mletele kueleza changamoto zinazowakabili ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kuomba kurasimishwa kwa mtaa wa Mlelewa na ukishasajiliwa uwe chini ya kata ya Seedfarm badala ya kupata huduma kiserikali katika kata ya Mletele ambako ni mbali na mtaa huo ili kukabiliana na tatizo la usumbufu wa upatikanaji wa huduma za kiofisi za Serikali, ukosefu wa huduma bora za kijamii kama vile vivuko na miundombinu ya umeme pamoja na kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi ya kata na mitaa yao ambapo Shaka ameahidi kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Songea.
Alihitimisha kwa kuwahamasisha wananchi kushiriki ipasavyo katika sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango madhubuti ya maendeleo kwa kupata takwimu sahihi za wananchi wake.
Shaka alitembelea uwanja wa Majimaji na kushuhudia mchezo wa mpira wa miguu uliokuwa ukiiendelea kati ya UVCCM Mkoa wa Ruvuma na UVCCM Mkoa wa Mjini Zanzibar na kutoa zawadi ya shilingi Laki Tano (Sh.5,00,000) kwa timu ya Mkoa wa Ruvuma na shilingi Milioni Moja (Sh.1,000,000) kwa timu kutoka Zanzibar.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa