Manispaa ya Songea imezindua rasmi zoezi la ugawaji dawa ya Usubi kwa kaya zote zilizopo ndani ya Manispaa ambapo ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika jamii ikiwemo na ugonjwa wa minyoo ya tumbo, matende, trakoma pamoja na kichocho.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 27 Agosti 2021 katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Songea na kuudhuriwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Songea Pendo Daniel, wataalamu wa afya pamoja na waandishi wa habari.
Pendo amewataka wahudumu wa afya waliochaguliwa na kupewa mafunzo juu ya namna ya kusimamia zoezi la ugawaji dawa kuhakikisha wanamfikia kila mwananchi ndani ya Manispaa ya Songea pamoja na kufanya kazi hiyo kwa uweledi na uaminifu kama walivyoelekezwa ’Alisisitiza’.
Pia ametoa rai kwa wananchi wote kutumia dawa hizo ili kujikinga na ugonjwa wa Usubi lakini pia kuzingatia usafi wa mwili kwa ujumla, matumizi sahihi ya choo na usafi wa mazingira pamoja na kuachana na dhana potofu zinazopotosha jamii kuhusiana na dawa hizo.
Kwa upande wake mratibu wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele Manispaa ya Songea Broad Komba amesema kuwa zoezi hilo la ugawaji dawa ya ugonjwa wa Usubi limeanza rasmi leo na linatarajiwa kumalizika tarehe 29 Agosti 2021.
Ameongeza kuwa dawa hizo zitatolewa kwa watu wote kwa kuzingatia kipimo maalumu cha urefu isipokuwa hazitatumika kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wakina mama wajawazito pamoja na wagonjwa mahututi.
Kwa mujibu wa tafiti za wataalamu wa afya, nchini Tanzania wananchi wote milioni 53 wapo hatarini kuambukizwa magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele na idadi ya watu milioni 5 tayari wameshaathirika kwa mojawapo ya magonjwa hayo”Komba alibainisha”.
Ugonjwa huu wa Usubi husababishwa na minyoo inayoitwa “Onchocerca Volvulus” ambayo inaenezwa na inzi weusi wadogo wanaokaa kando ya mito yenye maji yaendayo kasi na husababisha ngozi kuwasha au kuwa na mabaka mabaka mithili ya mamba au mjusi pamoja na upofu.
NA AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
27.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa