Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Ruvuma Kelvin Mapunda amewaongoza wajumbe wa ALAT Mkoa wa Ruvuma na kuwasili katika Mkoa wa KATAVI katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa lengo la kujifunza namna ya uendeshaji na usimamizi wa Biashara ya Kaboni.
Biashara ya kaboni Wilaya ya Tanganyika imelenga kuhifadhi Mazingira (Misitu), kulinda na Kuhifadhi Bioanuai zote muhimu na zilizo hatarini kutoweka Duniani (Sokwe mtu), kutunza vyanzo vya maji na Wanyamapori wengineo na kuwaletea Maendeleo endelevu kwa jamii inayozunguka au kuzungukwa na Misitu katika dhima ya kupambana na Mabadiliko ya tabia nchi na madhara yake.
Mradi huo umelenga kuziwezesha jamii kufanya shughuli za maendeleo za vijiji kupitia mapato yatokanayo na kuuza hewa ya kaboni baada ya kuhifadhi Misitu yao kwa kuzuia uharibifu au ukataji miti katika maeneo ya vijiji yaliyohifadhiwa na kusimamiwa kisheria na wanajamii wenyewe sambamba na kuboresha huduma kwa jamii pamoja na kuhusisha jamii katika uhifadhi na kunufaika moja kwa moja na faida za uhifadhi.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Ruvuma walipotembelea Mkoa wa Katavi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika iliyofanyika tarehe 03 Julai 2024 kwa lengo la kujifunza namna ya uendeshaji wa Biashara ya Kaboni.
Akizungumza mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Ruvuma Kelvin Mapunda amewataka wajumbe wa kamati ya ALAT Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanajifunza mafunzo hayo kwa umakini na kuhakikisha wanakwenda kutekeleza kwenye Halmashauri sambamba na kuhusisha jamii katika uhifadhi na kunufaika na uhifadhi.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Katavi Neemia James alisema “Biashara kaboni ilianza mwaka 2018 ukiendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Taasisi ya CARBON TANZANIA kwa kushirikiana na Mradi wa TUUNGANE kwa afya na Mazingira bora katika Wilaya ya Tanganyika ambapo Biashara hiyo inatekelezwa katika Vijiji nane (8) ambavyo ni Lugonesi, Mwese, Lwega, Bujombe, Kapanga, Katuma, Mpembe na Kijiji cha Kagunga yenye jumla ya ukubwa wa Hekta 216,944 za ardhi katika vijiji vyote vyenye jumla ya wakazi 34,242 wanaofaidika na mradi huo.”
Alisema ili uweze kufanikisha kuanzisha biashara ya kaboni inahitaji kutekeleza hatua zifuatazo ikiwemo na Vijiji kuwa na mpango wa matumizi bora ya Ardhi, uwepo wa msitu uliotengwa kwenye mpango wa matumizi ya ardhi, Uwepo wa tangazo la Serikali (GN), kwa misitu ya Serikali kuu na Halmashauri, Misitu kuwa na mipango ya usimamizi (forest Management plan) , hii inaweza kuandaliwa mchakato ukiwa unaendelea kuwa na uthibitisho wa umiliki wa msitu, kuwa na eneo la kutosha (kubwa ) angalau hekta 50, Msitu usiwe wa uvunaji na ulindwe usiharibiwe.
Wakieleza faida zinazopatikana kutokana na mradi huo ni amoja na Misitu iliyotengwa na vijiji hufyonza hewa chafu zinazozalishwa kutoka viwandani ambapo vyombo vya usafiri na wanyama hasa binadamu huchangia katika kupunguza kiwango cha kaboni kwenye anga pamoja na Misitu iliyohifadhiwa husaidia kutunza vyanzo vya maji vinavyohakikisha upatikanaji wa maji na mvua za uhakika.
Aidha Faida nyingine ni mgawanyo wa fedha Kiasi cha Shilingi bilioni nne (4,276,000,000) kilichopatikana katika awamu ya sita 6 na saba 7 ambacho kilikabidhiwa katika Vijiji nane (08) nufaika wa biashara ya kaboni ambapo Kati ya fedha hizo, Halmashauri ya Wilaya ilipokea Shs.427,600,000 sawa na 10% na Vijiji nufaika Shs. 3,600,000,000 sawa na 90% pia Uchangiaji mapato katika Halmashauri kupitia mapato ya ndani ambapo tangu mradi umeanzishwa Halmashauri imekusanya zaidi ya shilingi milioni mia nane ishirini na tano laki sita (825,600,000) sawa 10% ya mapato.
Aliongeza kuwa faida nyingine ni utoaji wa ajira kwa jamii ambapo jumla ya vijana (200) wameajiriwa kama askari walinzi wa misitu ya vijiji kwa ajira hiyo hulipwa posho ya shilingi laki tatu (300,000) kila mmoja kwa kila mwezi, Ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Katuma na ujenzi wa Zahanati 6 katika vijiji vya Lugonesi, Kapanga, Mpembe , katuma Kagunga na lwega ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, pamoja na Utoaji wa Bima za afya kwa wakazi wote waishio kwenye vijiji vya kaboni ambapo hadi Juni februari 2023 kaya 4400 sawa na watu 26273 walipatiwa bima za afya.
Miradi mingine ni Ujenzi wa vyumba vya madarasa 52 kwenye vijiji 8 vya Kaboni na katika shule 1, Ujenzi wa jengo la Utawala katika Shule ya Sekondari Mwese, Utoaji chakula kwa wanafunzi shule za Msingi, Ajira za mkataba kwa Walimu 22 katika shule za msingi ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa walimu, ambapo walimu hao hulipwa Shs. 300,000, pia ujenzi wa nyumba za Watendaji wa kijiji cha Lwega, Utoaji posho za madaraka kama motisha kwa Wenyeviti na Watendaji wa vijiji ambao hulipwa Shs.300,000 kwa Wenyeviti na Shs.200,000 kwa Watendaji wa vijiji kila mwezi. “Alibainisha”
Wakizungumza na chanzo hiki cha habari baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Ruvuma, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuanzisha mradi wa Kaboni ambao unanufaisha jamii, pia unaongeza mapato katika Halmashauri.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY.
MWANDISHI ALAT RUVUMA.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa