HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea iliyopo mkoani Ruvuma, inakadiriwa kuwa na idadi ya Watu 252,150 wakiwemo Wanaume 119,182 na Wanawake 132,968 kutokana na ongezeko la asilimia 4.4 kwa mwaka, Aidha ina jumla ya Kaya 61,930 kwa wastani wa watu 4.2 kwenye kila kaya.
Halmashauri ina jumla ya Mitaa 95, Kata 21 na Tarafa 2. Halmashauri ina jumla ya waheshimiwa madiwani 28, kati yao 21 ni wa kuchaguliwa, 7 ni wawakilishi Viti Maalum. Halmashauri inalo jimbo moja la uchaguzi ambalo Mbunge wake ni Mhe. Damas Ndumbaro na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jackline Ngonyani.
Halmashauri ina jumla ya watumishi 2,521 Kati ya mahitaji ya watumishi 3,142 na hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 621.
Mchumi Mkuu wa Manispaa ya Songea Raphael Kimary anazitaja shughuli muhimu za kiuchumi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuwa ni Kilimo na biashara ambapo Kilimo huchangia asilimia 75 ya pato la Halmashauri.
Anayataja mazao yanayowapatia wananchi Mapato makubwa ni Mahindi na Mpunga, aidha pato la mkazi wa Manispaa ya Songea ni 738,022.00 kwa mujibu wa ripoti ya GDP iliotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2006.
Kwa sasa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ipo katika hatua za mwisho za kukokotoa pato la mkazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kujua pato la mkazi kwa sasa.
Karoline Bernad ni Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea anasema Manispaa hiyo ina Mtandao wa barabara ulioingizwa kwenye mfumo wenye Jumla ya km 460.15. Kati ya hizo km 14.96 ni za lami, km 125.32 ni za changarawe na km 319.87 ni za udongo.
Mameritha Basike ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea anaeleza kuwa Halmashauri hiyo ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 35, ambavyo kati ya hivyo Hospitali ni moja Vituo vya Afya vitatu, na Zahanati ni 31.
Hata hivyo anabainisha kuwa Hospitali iliyopo ni hospitali ya rufaa ya Mkoa na kwamba Vituo vya Afya viwili vinamilikiwa na Serikali na kituo cha afya kimoja kinamilikiwa na shirika la dini, zahanati 17 zinamilikiwa na serikali.
Anabainisha zaidi kuwa zahanati mbili zinamilikiwa na Mashirika ya dini,tano zinamilikiwa na majeshi na zahanati saba zinamilikiwa na watu binafsi na kwamba kuna Kliniki tano zinazotoa huduma mbalimbali za afya katika manispaa hiyo.
’‘Halmashauri imeendelea kutekeleza ujenzi mbalimbali katika sekta ya Afya,ambapo kwa sasa kuna ujenzi wa kituo cha Afya kimoja na Zahanati nane. Mwaka wa fedha wa 2015/2016 Halmashauri iliweza kufungua zahanati mpya tatu, mwaka 2017/2018 zahanati mpya mbili, zilifunguliwa na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 vituo vipya vitano vinatarajiwa kufunguliwa’’,anasisitiza Dkt.Basike.
Anasema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 400,000,000 kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya Kata ya Ruvuma, hadi sasa shughuli za ujenzi wa kituo zinaendelea na ujenzi umefikia hatua ya msingi.
Hata hivyo anasema hali ya utoaji wa chanjo ni nzuri kwa sababu chanjo ya Penta tatu ambayo ndiyo kigezo cha mpango wa chanjo kitaifa ambayo umefikia asilimia 94,lengo la kitaifa ni kufikia asilimia 90 na kwamba Kiwango cha utapiamlo mkali ni asilimia 0.1 na utapia mlo usio mkali ni asilimia 4.1 Kuanzia mwanzoni mwa mwezi Januari 2017 hadi sasa hatuna upungufu wa chanjo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo Halmashauri imefanikiwa kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka asilimia 3.9 mwaka 2017 hadi asilimia 3.2 mwezi machi 2018.
Kulingana na Dkt.Basike,Huduma za Afya ya uzazi na mtoto zinatolewa katika vituo 29 na kwamba Huduma zinazotolewa ni chanjo kwa Watoto chini ya mwaka mmoja, huduma kwa wajawazito na wazazi ili kuzuia maambukizi ya Ukimwi toka kwa Mama kwenda kwa Mtoto ikiwemo ushiriki wa akina Baba.
“Vifo vya Wajawazito bado ni tatizo katika Halmashauri yetu kwani vifo hivyo vimeongezeka toka 182/10000 Mwaka 2016 hadi vifo 202/100,000 mwaka 2017. Bado jitihada za kupunguza vifo hivyo vya akina mama zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za upasuaji katika kituo chetu’’,anasema.
Anayataja Magonjwa yanayoongoza katika Manispaa ya Songea ni Malaria asilimia 34,magonjwa ya mfumo wa hewa ni asilimia 32.3,magonjwa ya njia ya mkojo(UTI) ni asilimia 11.2,Magonjwa ya ngozi asilimia 9.9,Magonjwa ya vichomi(Nimonia) asilimia 7.6 na magonjwa ya kuhara ni asilimia tano.
Kuhusu mapokezi ya dawa,Dkt.Basike anasema Manispaa ya Songea imekuwa ikipokea dawa na vifaa tiba toka serikali kuu kwa asilimia 91.1 hadi sasa. Hata hivyo amesema Halmashauri hununua dawa za nyongeza kufidia zile zinazokosekana MSD kupitia vyanzo vingine vya fedha ikiwemo Mfuko wa pamoja wa afya, Bima ya Afya, CHF na fedha za papo kwa papo.
Halmashauri ya Manispaa imekuwa ikitekeleza shughuli za Mfuko wa wa Afya ya jamii (CHF) tangu mwaka 2006 ambapo hadi kufikia machi 2018, kaya 7045 sawa na asilimia 11 ya kaya zote za Manispaa 60,036 zimejiunga na CHF.
Amesema utoaji wa vitambulisho bure kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 umefanyika kwa wazee 1,200 sawa na asilimia 10.9 lengo likiwa ni kuwafikia wazee 11,678 katika Kata zote 21. Pia Halmashauri imeingia mkataba na vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vinamilikiwa na Mashirika ya dini kutoa mitibabu bure kwa wazee 600.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa