WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema vivutio vya utalii vilivyopo katika ziwa Nyasa havipatikani katika sehemu nyingine yoyote Duniani hivyo serikali na wadau wengine wanatakiwa kufungua milango ya Utalii mwambao mwa ziwa hilo hali itakayovutia wawekezaji katika sekta ya Utalii .
Tanzania inashika nafasi ya pili Duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii,hata hivyo bado vivutio vingi havijaibuliwa na kuendelezwa .Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania, Malawi na Msumbiji, ziwa hilo lina urefu wa karibu kilometa 1000 na upana mkubwa wa kilometa 80 ambapo upana mdogo ni kilometa 15.
uwepo wa Ziwa Nyasa ambalo linapatikana Kusini – Magharibi mwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ziwa Nyasa ni la tisa kwa ukubwa duniani,ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika.
Ziwa hilo lina kina cha kati ya mita 426 na 758 na hii ni kutokana na kupitiwa na bonde la ufa. Kwa upande wa Tanzania mito mingi inapatikana ikitokea wilaya ya Nyasa katika safu za milima ya Livingstone, mito hiyo ni Ruhuhu, Lumeme, Ruhekei,Lwika,Mbamba Bay,Likumbo na Chiwindi ambayo huingiza maji ndani ya Ziwa Nyasa.
Kwa mujibu wa Afisa Maliasili na Utalii wa wilayani Nyasa,ziwa Nyasa ni kuvutio kikubwa cha Utalii kanda ya kusini kwa kuwa limesheheni vitu vingi ndani yake na tabia tofauti ukilinganisha na maziwa mengine ya hapa nchini na duniani kote.
“Baadhi ya tabia za ziwa hili ni uwepo wa maji meupe na maangavu eneo lote la ziwa na mawe marefu ambayo yanajulikana kwa majina ya hia na mala yanayobeba sifa tofauti’’,anasema Bugingo.
Tabia nyingine za Ziwa hilo anazitaja kuwa ni mawimbi makubwa, fukwe nzuri na zenye sifa tofauti, mawe kuonekana kama sakafu eneo la Chiwindi, fukwe zenye udongo wa mfinyanzi, kina cha maji kuwa kifupi kwa umbali mrefu na mchanga mdogo ambao watu wa kale walitumia kusugulia meno ili yawe meupe hasa katika fukwe za Mtipwili.
Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na SADC ziwa Nyasa lina kiasi cha tani 165,000 za samaki jambo muhimu hapa ni kuhakikisha vivutio vya utalii vilivyopo katika ziwa Nyasa vinatangazwa na kuendelezwa hali ambayo itachangia kuinua uchumi wa wiaya zinazozunguka ziwa hilo ikiwemo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa